City yaipa United ubingwa, Chelsea yaipiga Liverpool

MANCHESTER City, jana ilionyesha dhahiri kuwa Manchester United ni bingwa wa Ligi Kuu ya England baada ya kukubali kichapo cha aibu cha mabao 3-1 kwenye Uwanja wa White Hart Lane.
Kufungwa kwenye mchezo huo kunamaanisha kuwa leo Manchester United wana nafasi kubwa ya kutangazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya England ikiwa wataibuka na ushindi katika mechi dhidi ya Aston Villa.
United leo inavaana na Aston Villa na kama watashinda basi watakuwa mabingwa wa England kwa mara ya 20.
City ambao ni mabingwa watetezi wamebaki na pointi 68 na kama United watashinda watakuwa na pointi 84 ambazo hakuna timu nyingine yoyote kwenye ligi kuu msimu huu inaweza kuzifikia.

City ndiyo walikuwa wa kwanza kupatia bao lililowekwa kimiani na kiungo, Samir Nasri, katika dakika ya tano tu ya mchezo huo.
Spurs ambayo kama ingepoteza mchezo huo ingekuwa kwenye nafasi mbaya ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ilicharuka kipindi cha pili na kupata mabao ya haraka.
Katika dakika ya 75, Clint Dempsey aliifungia timu hiyo bao la kusawazisha kwa ufundi wa hali ya juu. Dakika nne baadaye Jermain Defoe ambaye aliingia kipindi cha pili aliifungia bao la pili kwa shuti kali na kuwamaliza kabisa City.
Hata hivyo, wakati vijana wa Kocha Roberto Mancini, wakijitahidi kwa nguvu zote kupata bao la kusawazisha Gareth Bale ambaye alitokea kwenye benchi alifunga bao la tatu.
Katika mchezo mwingine uliopigwa jana, Liverpool ikiwa nyumbani ilijikuta ikiilazimisha Chelsea na kwenda nayo sare ya mabao 2-2.
Chelsea ilikuwa ya kwanza kupata bao, shukrani kwa Oscar aliyefunga katika dakika ya 26.
Daniel Sturridge aliifungia Liver bao kusawazisha katika dakika ya 52, lakini dakika tano baadaye Eden Hazard akaifunga Chelsea bao la pili kwa mkwaju wa penalti.
Wakati Chelsea wakiamini kuwa wanaondoka na pointi tatu kwenye Uwanja wa Anfield, Liverpool walipambana na kusawazisha katika dakika ya 96 ya mchezo kwa bao safi la Luis Suarez.

0 commentaires:

Sema Tunakuskia na wewe